Soka ya wanaume kwa sasa imekuwa ikikua kwa kasi zaidi ikilinganishwa na ile iliyokuwa ikichezwa tangu miaka ya 1900. Mabadiliko makubwa yameonekana kwa upande wa kiteknolojia na kuiboresha kibiashara kwa kuunda ligi zenye vilabu na timu bora duniani mfano La Liga, Ligi za Afrika, UEFA, Ligi ya premia n.k.
Lakini swali la kujiuliza ni nini hasa kinasababisha soka ya wanawake kuwa nyuma ikilinganishwa na soka ya wanaume? Nafikiri jibu la moja kwa moja ni kwamba soka ya wanawake imeanza kufuatiliwa na wanawake ama wadau soka katika miaka si ya zamani sana ikilinganishwa na soka ya wanaume, na hii ni kutokana na kwamba hapo awali ilionekana mtoto wa kike kucheza soka ni kama uhuni. Hata hivyo kadiri siku zinavyokwenda mbele, watu wa mataifa mbalimbali walitambua kuwa hata wanawake pia wanafaa kucheza soka, na wala sio jambo baya kwao.
Tumeshuhudia wanaume nao wakicheza michezo mingi ambayo hapo awali ilitambulika kama michezo ya wanawake tu, mfano mpira wa pete, sasa kuna mashindano mbalimbali ya mpira wa pete kwa wanaume. Kwa hiyo sio vibaya na kwa upande wa wanawake nao kujikita kwenye michezo ambayo wanaweza kuicheza kwa mfano soka. Ndio maana leo kwenye kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake tutazungumzia juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na wadau wa soka katika kukuza soka ya wanawake.