Mkuu wa UNHCR asisitiza kujitolea kusaidia wakimbizi nchini Ethiopia
2023-02-10 09:52:20| CRI

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) Bw. Filippo Grandi amesisitiza dhamira ya kuunga mkono mwitikio wa kibinadamu kwa wakimbizi na wale waliopoteza makazi yao nchini Ethiopia na kujitahidi kufikia suluhu ya muda mrefu, ikiwa ni pamoja na wale waliokimbia makazi yao kutokana na ukame na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Bw. Grandi amesema hayo alipohitimisha ziara yake ya siku tatu nchini Ethiopia, ambapo alikutana na maafisa waandamizi wa serikali na watu waliopoteza makazi yao wakiwemo wakimbizi wa Eritrea.

Taarifa iliyotolewa na UNHCR imesema kuwa tangu kufikiwa kwa makubaliano ya amani mwezi Novemba mwaka jana, UNHCR na washirika wengine wameweza kuongeza kasi ya utoaji wa misaada inayohitajika ikiwa ni pamoja na dawa, vifaa vya makazi, nguo, vifaa vya nyumbani na mablanketi.