Mtafiti kutoka kampuni ya ushauri ya Knight Frank nchini Kenya, Boniface Abudho amesema, wajenzi kutoka China na miradi ya miundombinu inayojengwa nao inachukua nafasi muhimu katika ukuaji wa sekta ya mali zisizohamishika barani Afrika.
Akizungumza na Shirika la Habari la China Xinhua mjini Nairobi, Bw. Abudho amesema, miradi ya miundombinu ya reli na barabara iliyotekelezwa na wajenzi kutoka China imefungua maeneo mengi na kuwezesha watu kutoka kwenye maeneo ya msongamano mijini na kuhamia kwenye miji midogo ya pembezoni.
Pia amesema, wajenzi kutoka China wameshiriki katika miradi mikubwa ya ujenzi wa nyumba, na hivyo kusaidia watu kupata nyumba kwa gharama nafuu.
Naye mtafiti mwandamizi kutoka kampuni hiyo Charles Mwangi amesema, wajenzi kutoka China wametekeleza miradi mingi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ambazo zitaisaidia Kenya kuondoa pengo la uhaba wa nyumba kwa kuongeza upatikanaji wa nyumba bora.