Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kiwango cha 4.7 limetokea umbali wa kilomita 33 kutoka visiwani Pemba na kusikika katika baadhi ya miji nchi ya Tanzania na Kenya, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imethibitisha.
Mawimbi ya tetemeko hilo yamedaiwa kusikika jumatano majira ya saa 12:30 jioni, huku baadhi ya wakazi wa jiji la Tanga nao wakieleza kuwa walilihisi tetemeko hilo.
Tetemeko hilo linalodhaniwa kutokea katikati ya Bahari ya Hindi limekuja ikiwa ni siku mbili tangu tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.8 kuathiri nchini Uturuki ambapo maelfu ya watu wamepoteza maisha yao na kujeruhiwa, na majengo na miundombinu kadhaa kuharibiwa.