Mkuu wa mkoa wa Dodoma Bibi Rosemary Senyamule amesema watu 12 walifariki na wengine 63 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea Jumatano usiku huko wilayani Kongwa mkoani Dodoma, katikati mwa Tanzania.
Senyamule alisema basi moja lililokuwa likitokea Dar es Salaam na kuelekea Bukoba wilayani Kagera liligongana uso kwa uso na lori lililosafirisha saruji Jumatano usiku katika kijiji cha Silwa kilichoko kando ya barabara kati ya Dodoma na Morogoro. Wanaume wanane na wanawake wanne waliokuwemo ndani ya basi walikufa papo hapo, na majeruhi 63 walikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Silwa.