Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo ameongoza zoezi la ufungaji visukuma mawimbi ‘GPS Satellite’. Collars" kwa makundi ya Tembo wanaosumbua wananchi katika Vijiji vya Wilaya za Nachingwea, Liwale na Tunduru.
Zoezi hilo linaloendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), pamoja na viongozi wa Wilaya na vijiji lilianza kutekelezwa Februari 10, 2023. Lengo ni kusaidia kupata taarifa kwa wakati kuhusu mienendo na mahali yalipo makundi ya tembo na hivyo kurahisisha ufuatiliaji na kuzuia wanyamapori hao wasilete madhara kwa watu, makazi na mashamba yao.
Katika zoezi hilo jumla ya visukuma mawimbi vitano vilitarajiwa kufungwa kwenye makundi ya tembo, ambapo hadi kufikia Februari 12, 2023 jumla ya visukuma mawimbi vitatu vilifungwa kwenye makundi matatu ya tembo katika maeneo ya Milola/Mitamba (Wilaya ya Lindi vijijini), Mkutano (Liwale) na Ngolanga ambayo ni shoroba ya Selous - Niassa (Tunduru). Visukuma mawimbi viwili vilivyobaki vinatarajiwa kufungwa katika maeneo ya Wilaya hiyo yenye changamoto kubwa zaidi.