Marekani yapaswa kuacha mashaka ya kupita kiasi kuhusu China
2023-02-14 09:50:04| CRI

Hivi karibuni puto moja la uchunguzi wa hali ya hewa la China ambalo lilifika Marekani kwa bahati mbaya limefuatiliwa sana na Wamarekani. Kutoka kugundua puto hilo tarehe Mosi hadi kuiliangusha kwa makombora tarehe 4 mwezi huu, baadhi ya wanasiasa wa Marekani wametumia fursa hiyo kuchochea wazo la “Matishio ya China”. Hata waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo ameahirisha ziara yake aliyokuwa afanye nchini China.

Puto hilo lililoonekana juu ya anga nchini Marekani ni puto la kiraia la China la utafiti wa kisayansi wa hali ya hewa, ambalo lilipepea hadi Marekani kutokana na upepo wa magharibi, na kwa wakati mwingi limekuwa zaidi ya mita 40,000 juu ya ardhi. Baada ya tukio hilo kutokea, China ilitoa ufafanuzi wa wazi, na kuiambia Marekani kuwa, ingawa puto hilo lilitoka China, lakini ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia, na China itaendelea kudumisha mawasiliano na Marekani ili kushughulikia tukio hilo. Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya China Wang Yi, pia amesisitiza kuwa, China ni nchi inayowajibika na inafuata sheria za kimataifa siku zote, nchi hizo mbili zinapaswa kuwasiliana kwa wakati ili kushughulikia vizuri tukio hilo lisilotarajiwa.

Puto hilo ni kubwa sana kiasi kwamba linaweza kuonekana kwa macho ya kawaida wakati linapokuwa mita 40,000 angani. Lakini kwa uhusiano wa China na Marekani, puto hilo ni kituo kidogo mno. Kusema kweli, matukio ya maputo ya kiraia kuvuka mpaka ni mambo ya kawaida, na hata maputo ya uchunguzi ya Marekani yameonekana angani nchini China mara nyingi. Kulingana na Makubaliano ya Geneva, vyombo vya kuruka vya kiraia vikipotea katika eneo la nchi nyingine, hutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia. Hata hivyo, safari hii haikuwa hivyo kwa Marekani, ambayo hatimaye ilitumia ndege yake ya kijeshi aina ya F22 kuangusha puto hilo.

Mara baada ya Marekani kugundua puto hilo, waliambiwa na China kuwa hilo ni puto la kiraia. Hata hivyo baada ya puto hilo kufika nchini Marekani na kuonekana na watu wa nchi hiyo, ghafla serikali ya Marekani ilidai kuwa puto hilo ni la kijasusi, na ni hatari sana. Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilisema puto hilo lilikuwa likijaribu kuchunguza eneo la kurusha makombora ya nyuklia. Hata hivyo, jeshi la Marekani liliruhusu puto hilo kuendelea kuruka kwenye nchi hiyo bila kuchukua hatua yoyote. Kwani hii ni fursa nzuri sana kwa serikali ya Marekani na wanasiasa kueneza wazo la “matishio ya China”. Vyombo muhimu vya habari vya Marekani, ikiwa ni pamoja na CNN na Fox News, vimeendelea kuripoti puto hilo, ili kuongeza uhasama wa Wamarekani kwa China.

Lakini ukweli ni kwamba, puto halifai kwa kazi ya ujasusi. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mtandao wa Habari wa “Politician” wa Marekani, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeendelea na utafiti wa maputo ya kijasusi kwa karibu miaka 30, mwishowe, ilitambua kuwa kazi hiyo inafaa zaidi kufanywa na satelaiti za obiti za chini. Wataalamu wanaona kuwa haiwezekani kwa China kutofahamu hilo kiasi cha kurusha puto kubwa namna hiyo kwenda nchini Marekani, na kutarajia kutogunduliwa. Gazeti la Washington Post hivi karibuni lilisema, hata kama puto hilo la China halina uwezo wa kuchunguza Marekani, limeleta wasiwasi kwa Wamarekani.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imezidi kuichukulia China kama mshindani wake mkuu, na baadhi ya wanasiasa wa nchi hiyo wamejitahidi sana kutetea wazo la “matishio ya China”. Hata hivyo, ukiwa uhusiano muhimu zaidi kati ya nchi mbili duniani, uhusiano kati ya China na Marekani si kama tu unahusisha maslahi ya nchi hizo mbili, bali pia una athari kubwa kwa dunia nzima. Marekani inapaswa kuondoa mashaka yake makubwa kuhusu China, na kushughulikia matukio yasiyotarajiwa na China kwa njia ipaswavyo.