EU yaondoa marufuku ya mamung'unye machungu yanayolimwa Tanzania
2023-02-14 21:42:09| cri

Umoja wa Ulaya (EU) umeondoa marufuku ya mamung'unye machungu “bitter gourd” yanayolimwa Tanzania kuingia kwenye masoko yake yenye faida kubwa, na hivyo kuwapa faraja wakulima na wauzaji bidhaa nje ya nchi.

Novemba 2022, EU iliripoti kuwa iligundua uwepo wa wadudu wa karantini katika matunda hayo ambayo kitaalamu yanayojulikana kama MomordicaCharantia, na kusababisha Tume ya Ulaya kupiga marufuku uuzaji wa zao hilo katika masoko ya EU, na kuathiri sana sekta hiyo kwa mamilioni ya shilingi.

Tanzania ikiwa mzalishaji wa mamung'unye machungu, kati ya Januari 2021 na Julai 2022 iliuza nje takriban tani 220 za mazao hayo kwenda Uingereza, Uholanzi, Italia, Ubelgiji na Uswisi, na kuingizia uchumi kiasi cha dola za Kimarekani 691,000 (karibu TSH 1.5bn/-). Tanzania ilitakiwa kuwasilisha mbele ya EU ripoti ya uchunguzi wa wadudu kuthibitisha kutokuwepo kwa ThripspalmiKarny ili iruhusiwe kusafirisha matunda hayo kwenye masoko ya EU.