Makubaliano ya Amani ya Sudan hatarini kutokana na uhaba wa fedha na mvutano wa kisiasa
2023-02-14 08:39:09| CRI

Utekelezaji wa Makubaliano ya Amani yaliyosainiwa Agosti 2020 kumaliza mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa nchini Sudan umesitishwa kutokana na mvutano wa kisiasa na ukosefu wa uungaji mkono wa kimataifa.

Hayo yamesemwa na wapatanishi wa makubaliano hayo jana jumatatu wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku tano kutathmini makubaliano hayo ya amani linalofanyika mjini Juba, Sudan Kusini.

Waziri wa Uwekezaji wa nchini Sudan Kusini, ambaye ni mjumbe wa timu ya upatanishi, Dhieu Mathok Diing amesema, mvutano wa kisiasa unaoendelea uliotokana na kutokubaliana kuhusu uongozi wa pamoja kati ya makundi yaliyosaini makubaliano hayo unaathiri utekelezaji wake.

Katibu mkuu wa kundi la SPLM-N la mkoa wa Blue Nile, Salwa Adam amesema, hali ya kisiasa nchini Sudan imeathiri utekelezaji wa Makubaliano ya Amani kwa kuwa hakuna serikali halali kwa sasa nchini humo.

Mwenyekiti wa Tume ya Amani ya Sudan, Suliman Mohammed Dibelo ameeleza matumaini yake kutokana na mfumo wa makubaliano uliofikiwa hivi karibuni kati ya Baraza la Utawala la Sudan na makundi ya upinzani.