Rais Xi Jinping wa China amefanya mazungumzo na mwenzake wa Iran Ebrahim Raisi ambaye yupo ziarani nchini China mjini Beijing.
Katika mazungumzo hayo, rais Xi amesema, China siku zote inachukulia uhusiano wake na Iran kwa mtazamo wa kimkakati, na kwamba China itashikilia kithabiti kukuza ushirikiano wa kirafiki na Iran, kuhimiza uhusiano wa wenzi wa kimkakati kati yake na Iran katika pande zote kupata maendeleo mapya, ili kuchangia katika amani ya dunia na maendeleo ya binadamu.
Kwa upande wa rais Raisi amesema, Iran inaunga mkono kithabiti pendekezo la China la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, pamoja na mapendekezo ya maendeleo na usalama ya dunia. Pia Iran inapenda kuimarisha mawasiliano na China katika masuala ya kimataifa na kikanda, ili kulinda usawa na haki ya kimataifa na amani na usalama wa kikanda na dunia nzima.
Baada ya mazungumzo hayo, marais hao wawili walishuhudia kusainiwa kwa nyaraka za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta za kilimo, biashara, utalii, ulinzi wa mazingira, afya, uokoaji wa maafa, utamaduni na michezo.