Kenya yaongeza ulinzi kukabiliana na ujangili katika eneo la kaskazini mashariki
2023-02-14 08:39:49| CRI

Rais wa Kenya William Ruto ameamuru operesheni kubwa ya usalama ifanyike ili kukusanya silaha haramu kwa lengo la kupunguza ujangili ambao umeongezeka katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Rais Ruto amesema, zoezi la siku tatu la kusalimisha silaha kwa hiari, litakalofanywa kwa pamoja na vikosi vya usalama kutoka Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi (KDF), litawapa watu wa eneo hilo muda wa kusalimisha silaha zao.

Kauli ya rais Ruto imekuja wakati idadi ya vifo vinavyotokana na ujangili katika kaunti za Baringo, Elgeyo Marakwet, Turkana na Pokot Magharibi ikiongezeka na kuzidi watu 40 ndani ya mwezi mmoja, wakati serikali ikiimarisha usalama ili kudhibiti uhalifu huo.

Katika shambulizi la karibuni, askari polisi wanne walikuwa miongoni mwa watu 10 waliouawa kwenye shambulizi la majangili katika barabara kuu ya Kitale-Lodwar katika kaunti ya Turkana lililotokea ijumaa iliyopita.