Mkutano wa 6 wa Uvumbuzi na Teknolojia Endelevu Duniani wafanyika huko Rio de Janeiro, Brazil
2023-02-14 18:43:08| cri

Mkutano wa 6 wa Uvumbuzi na Teknolojia Endelevu Duniani (G-STIC), umeanza tarehe 13 na utaendelea hadi tarehe 15 mwezi huu huko Rio de Janeiro, Brazil.

Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika katika nchi ya Amerika Kusini. Mkutano huu wa siku tatu unazingatia na kujadili mada mbalimbali zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, anuai ya viumbe hai, uchafuzi wa mazingira, kujenga upya ulimwengu wenye afya zaidi baada ya janga la COVID- 19 na kadhalika.

Waziri mpya wa afya wa Brazil Bibi Nísia Trindade Lima alitoa hotuba katika ufunguzi wa mkutano huu ambapo viongozi na wanasayansi wengi kutoka mashirika ya kimataifa walishiriki kwenye ufunguzi huo.

Mkutano wa kwanza wa G-STIC ulifanyika huko Brussels mwezi Oktoba mwaka 2017 na toka hapo umekuwa ukifanyika kila mwaka na kuweka ajenda inayohusu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya 2030.