Tutokomeze ukeketaji
2023-02-17 08:00:50| CRI

Tarehe 6 Februari ya kila mwaka ni Siku ya Kupinga Ukeketaji, na siku hii ilianza kuadhimishwa mwaka 2003 ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kuwa siku rasmi ya kimataifa ya kupinga ukeketaji duniani kote. Ukeketaji ni moja ya madhila anayokumbana nayo mtoto wa kike na mwanamke kutokana na mila ambazo ni potofu, mila ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike na mwanamke, mila ambazo zinawadhalilisha kijinsia watoto wa kike, wasichana na wanawake.

Takwimu zinaonyesha kuwa, watoto wa kike na wanawake milioni 200 wamefanyiwa kitendo hiki cha kikatili, na nusu yao wakitokea nchi za Misri, Ethiopia, Indonesia, huku nchi za Somalia, Guinea na Djibouti zikiwa na idadi kubwa ya wanawake waliokeketwa barani Afrika. Ingawa elimu imekuwa ikitolewa kuhusu athari za kitendo ama mila hii, lakini bado watoto wa kike na wanawake wamejikuta wakifanyiwa kitendo hiki bila hata ya ridhaa yao. Mbaya zaidi, kutokana na ukeketaji kupigwa marufuku, hivi sasa wanaofanya kitendo hicho wamebuni njia mpya, ambapo mtoto wa kike anakeketwa pindi anapozaliwa. Basi katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutazungumzia suala hili la ukeketaji na nini kifanyike kumaliza ama kuondokana na mila hii.