Benki ya Dunia yasema uchumi wa Tanzania wazidi kuimarika
2023-02-15 22:20:16| cri

Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania inaonesha kuwa pato la Tanzania linatarajia kupanda kutoka asilimia 4.6 za mwaka jana hadi asilimia 5.3 mwaka huu.

Sehemu ya ripoti hiyo iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam imetaja sababu zilizochangia kukua kwa uchumi wa Tanzania ni kufunguliwa kwa shughuli za utalii, mipaka kwa shughuli za kiuchumi na mafanikio kwenye chanjo dhidi ya COVID-19, hali iliyofungua nyanja za biashara na uzalishaji.

Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imesifu misingi ya kiuchumi ya Tanzania kuhimili misukosuko ya kiuchumi iliyoziumiza nchi nyingi za Afrika kutokana na janga la COVID-19 ambalo lilizorotesha uchumi wa nchi za kusini mwa Sahara.

Hata hivyo ripoti hiyo imesema mlipuko wa COVID- 19 ulisababisha kiwango cha umaskini kuongezeka kutoka asilimia 21 mwaka 2019 hadi asilimia 26 mwaka 2021 kwa nchi nyingi za kusini mwa Sahara, ikiwa ni pamoja na Tanzania.