Tanzania imetajwa kuendelea kuwa katika njia sahihi kiuchumi, huku asilimia ya ukuaji ikiongezeka mwaka hadi mwaka, kutokana na maendeleo ya sekta ya kilimo na huduma kwa upande wa ugavi na uwekezaji.
Ukuaji wa Pato la Taifa ulikadiriwa kuwa asilimia 5.0 na asilimia 5.6 mwaka 2022 na 2023, kutokana na kuboreshwa kwa utendaji katika sekta za utalii, kufunguliwa tena kwa njia za biashara na kuharakishwa kwa utoaji wa chanjo ili kukabiliana na janga la COVID-19.
Benki ya Dunia (WB) imenukuliwa ikisema kuwa jumla ya deni la Tanzania, ambalo linahusisha sekta binafsi, bado ni dogo ikilinganishwa na pato la Taifa.
Ripoti ya Benki hiyo kuhusu uchumi wa Tanzania imeonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na hatari ya kati dhidi ya deni la nje. Ripoti imesema serikali inatakiwa kupongezwa kwa kuweza kudumisha sera nzuri na kutekeleza mpango wa maendeleo.