Zaidi ya wapiganaji 200 wa kundi la al-Shabab wameuawa katika operesheni ya wiki moja iliyofanywa na jeshi la Somalia kwa kushirikiana na vikosi vya kikanda katika mikoa ya kusini na katikati ya Somalia.
Waziri wa Habari wa nchi hiyo Daudi Aweis Jama amewaambia wanahabari jana mjini Mogadishu kuwa, operesheni ya hivi karibuni dhidi ya kundi hilo lenye uhusiano na kundi la Al-Qaida imefanikiwa, ambapo askari waliongeza mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa al-Shabab katika maeneo yaliyoko mikoa ya Galmudug, Hirshabelle, Kusini Magharibi na Jubbaland.
Amesema wapiganaji wengi walijisalimisha wakati wa mapigano hayo, akiwemo kamanda wa kundi hilo na mtaalamu wa mabomu.