Kamishna wa Maendeleo ya Uchumi, Biashara, Viwanda na Madini wa Umoja wa Afrika, Albert Muchanga amesema, bara la Afrika haliwezi kuacha kutekeleza makubaliano ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA).
Akizungumza na wanahabari wakati wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Utendaji unaofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, Bw. Muchanga amesema Eneo hilo ni ufunguo muhimu katika mageuzi ya Afrika, na kushindwa kutekeleza mradi huo ni jambo lisiloweza kufikirika.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ni safari ndefu na italisaidia bara la Afrika kutimiza soko la kikanda kwa uhuru wa watu kusafiri, mitaji, bidhaa na huduma ili kuimarisha maingiliano ya kiuchumi, kuboresha maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula, mageuzi ya viwanda na mabadiliko ya mfumo wa uchumi.