Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia miundombinu na nishati Bi. Amani Abou-Zeid, amezihimiza nchi za Afrika kubadilisha changamoto kuwa fursa za kuleta mageuzi kwenye sekta ya nishati ya Afrika.
Akikutana na wanahabari kando ya kikao cha 36 cha kawaida cha mkutano wa Umoja wa Afrika, Bi Abou-Zeid amesema miaka mitatu iliyopita ilikuwa migumu duniani ikiambatana na mfululizo wa misukosuko ambayo imeleta uharibifu katika uchumi na maisha ya watu.
Amesema Umoja huo ukishirikiana na wenzi wake wamefanya juhudi ili kulifanya bara la Afrika kurejea katika njia ya ufufukaji baada ya janga la COVID-19.
Amesema ukosefu wa nishati uliokuwepo kwa muda mrefu barani Afrika unazidi kuwa mbaya, akisisitiza haja ya kufanya juhudi kukabiliana na changamoto hiyo, na kwamba kuna haja ya kuboresha maendeleo na matumizi ya nishati safi na endelevu barani humo.