Zaidi ya vyandarua 500,000 kugawiwa kwa wanafunzi wa mkoa wa Tanga nchini Tanzania
2023-02-20 08:59:13| CRI

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Omary Mgumba amesema jumla ya vyandarua laki 5.29 vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.9 za Tanzania vitagawiwa kwa wanafunzi wa shule 1,083 za msingi katika mkoa wa Tanga.

Akiongea wakati wa kuanza kwa ugawaji wa vyandarua hivyo, Bw. Mgumba amesema kugawa vyandarua hivyo kunalenga kuwasaidia wanafunzi wa shule za msingi kujikinga dhidi ya maambukizi ya Malaria, na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 45.

Bw. Mgumba alisema ugawaji wa vyandarua hivyo unaratibiwa na serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Amewataka viongozi wa jumuiya kusimamia ugawaji wa vyandarua katika maeneo yao.