China kudumisha mazingira ya biashara ya kimataifa yaliyo wazi na yenye utaratibu
2023-02-20 08:23:09| CRI

Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China Bw. Wang Yi amesema China inapenda kushirikiana na Ubelgiji katika kudumisha kithabiti mazingira ya biashara ya kimataifa yaliyo wazi na yenye utaratibu.

Bw. Wang Yi amesema hayo alipokutana na Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bw. Alexander De Croo kando ya Mkutano wa 59 wa Usalama wa Munich.

Bw. Wang amesema uhusiano kati ya China na Ubelgiji umedumisha mwelekeo mzuri wa maendeleo, ambapo biashara kati ya nchi hizo mbili imeweka rekodi mpya na ushirikiano wa kunufaishana kati yao pia umezaa matunda mapya, hali inayoendana na maslahi ya nchi zote mbili na inachangia maendeleo ya uhusiano kati ya China na Ulaya.

Bw. De Croo amesema Ubelgiji na China zimedumisha mawasiliano ya karibu akisisitiza kuwa nchi yake inatilia maanani uhusiano na China na itashikilia kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja.