Jitihada za kujiunga tena na Umoja wa Afrika (AU) za nchi tatu za Afrika Magharibi, ambazo bado ziko chini ya utawala wa kijeshi, ziligonga mwamba siku ya Jumapili baada ya jumuiya yao ya kikanda Ecowas, kuendeleza vikwazo ilivyoziwekea.
Nchi hizo tatu, zikiwa chini ya uongozi wa kijeshi kwa zaidi ya mwaka mmoja zilitoa hoja mbele ya viongozi wa Umoja wa Afrika siku ya Alhamisi, zikieleza haja ya kuondolewa katazo dhidi ya nchi hizo kushiriki kwenye Umoja wa Afrika.
Kwa kawaida, Umoja wa Afrika husimamisha nchi ambazo zinapitia mabadiliko ya kikatiba katika serikali kama vile mapinduzi hadi pale zitakapotoa mpango wa kawaida wa kurejesha uongozi wa kiraia. Lakini AU mara nyingi hufuata maamuzi ya jumuiya za kikanda ambazo zinafanya kazi kama watoa huduma ya kwanza.