Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, walinzi wa amani wa Umoja huo nchini Sudan Kusini wanafanya doria ili kuunga mkono makubaliano ya amani ya mwaka 2018 kati ya pande zinazopingana nchini humo.
Dujarric amesema, katika mkoa wa Ikweta Mashariki, walinzi wa amani wameongeza uwezo wa jamii za huko, hususan vijana, kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani. Ameongeza kuwa, walinzi hao wa amani pia wanafanya doria katika eneo kati ya Tseretenya na Ikotos ili kupunguza mivutano kati ya jamii za huko na kuboresha usalama.
Wakati huohuo, Dujarric amesema, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa pamoja na wenza wake wa maendeleo, limeomba jumla ya dola za kimarekani bilioni 1. 3 ili kulinda na kusaidia wakimbizi milioni 2.2 wa Sudan Kusini wanaoishi katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda.