Umoja wa Mataifa walaani shambulizi dhidi ya walinzi wa amani wa Umoja huo nchini Mali
2023-02-22 10:20:06| CRI

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulizi dhidi ya askari wa kulinda amani wa Umoja huo nchini Mali lililotokea jana jumanne na kusababisha vifo vya askari watatu wa kulinda amani kutoka Senegal na wengine watano kujeruhiwa.

Katika taarifa yake, nchi wajumbe wa Baraza hilo wametoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na kwa taifa la Senegal, na pia kuwatakia majeruhi wapone haraka.

Baraza hilo limeitaka serikali ya mpito ya Mali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu shambulizi hilo kwa kushirikiana na Tume ya Ulinzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA), kuongeza uwajibikaji kwa kuwafikisha wahusika mbele ya sheria, na kutoa taarifa kwa Tume hiyo juu ya maendeleo ya uchunguzi huo.