Sudan Kusini yasema vikwazo vya silaha vinakwamisha utekelezaji wa makubaliano ya amani
2023-02-22 08:49:28| CRI

Waziri wa habari, teknolojia za mawasiliano na huduma za Posta wa Sudan Kusini Bw. Michael Makuei Lueth, amesema vikwazo vya silaha ilivyowekewa Sudan Kusini vinakwamisha utekelezaji wa makubaliano yaliyohuishwa ya kutatua mgogoro wa Sudan Kusini (R-ARCSS).  

Bw. Makuei amesema serikali imekamilisha mafunzo ya kikosi cha pamoja bila kuwa na silaha, lakini watapowekwa kwenye maeneo mbalimbali watashindwa kuhakikisha usalama kutokana na kutokuwa na silaha.

Sudan Kusini imekamilisha mafunzo kwa vikosi vyake vyenye jumla ya askari elfu 52 wa vikosi mbalimbali ikiwa ni pamoja na polisi, idara ya usalama wa taifa, ulinzi wa wanyamapori, magereza, ulinzi wa viongozi na ulinzi wa kiraia, lakini hadi sasa hawajapelekwa kwenye maeneo ya kazi kutokana na kutokuwa na silaha.

Bw. Makuei ametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo hivyo ili Sudan Kusini iweze kuwapanga askari hao na kutekeleza makubaliano hayo kwa haraka.