Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imelaani vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi kwa Zimbabwe, ikisema hatua hiyo imesababisha mlundikano wa malipo ya ziada na deni la nje la Zimbabwe kwa miaka mingi.
Mkuu wa Benki hiyo, Akinwumi Adesina aliyeteuliwa na rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kufanya kazi kama mtetezi wa nchi hiyo katika mchakato wa maafikiano ya malipo ya ziada na deni hilo, amesema hayo mjini Harare alipokutana na wadai ili kukabiliana na deni hilo.
Amesema ingawa malipo kidogo yanafanyika ili kulipa deni hilo, lakini huu ni wakati wa kumaliza malipo yote ya ziada, kutatua na kupanga upya malipo ya deni hilo kwa ajili ya Zimbabwe.
Zimbabwe inadaiwa dola za kimarekani bilioni 14.04 na wakopeshaji wa kimataifa, huku deni linalodaiwa na wakopeshaji wa pande mbili likikadiriwa kufikia dola za kimarekani bilioni 5.75, na deni la wakopeshaji wa pande nyingi likikadiriwa kufikia dola za kimarekani bilioni 2.5.