China yatoa wito wa kurejesha mazungumzo ya amani ili kutatua mgogoro wa Ukraine
2023-02-24 13:25:18| CRI

China imetoa wito wa kufanyika juhudi za kimataifa ili kuweka mazingira ya kurejesha mazungumzo ya amani kwa minajili ya kutatua mgogoro wa Ukraine.

China leo Ijumaa imetoa waraka ukifafanua msimamo wake juu ya ufumbuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Ukraine, ukisema mazungumzo ni njia pekee mwafaka ya kutatua mgogoro huo.

Waraka huo umesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuhimiza mazungumzo ya amani, kuzisaidia pande zinazohusika na mgogoro huo kufungua mlango wa kutafuta suluhisho la kisiasa haraka iwezekanavyo, na kuweka mazingira ya kurejesha mazungumzo. China itaendelea kubeba jukumu la kiujenzi katika suala hilo.

Waraka huo pia umesema pande zote lazima zidumishe mantiki na kujizuia, kuepuka kuchochea mgogoro na kuongeza mvutano, na kuzuia mgogoro huo kuzidi kuwa mbaya na kutodhibitiwa.

Waraka huo umeongeza kuwa China inapinga mashambulizi dhidi ya vinu vya nyuklia au vituo vingine vya amani vya nyuklia, na kwamba tishio au matumizi ya silaha za nyuklia vinapaswa kupingwa, na ni lazima kuzuia kuenea kwa nyuklia na kuepuka mgogoro wa nyuklia.