WMO: Ukame utaendelea katika pembe ya Afrika
2023-02-24 09:18:04| CRI

Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limeonya kuwa matokeo ya maafa yanayotokana na ukame uliodumu kwa miaka kadhaa yataendelea mwaka huu katika kanda ya pembe ya Afrika, na kufanya jamii mbalimbali kukabiliana na mahitaji ya dharura ya msaada.

WMO imetoa taarifa ikisema kwa mujibu wa utabiri mpya wa kimajira, mvua ya kiwango cha chini kuliko kawaida inatarajiwa kunyesha katika sehemu nyingi za kanda hiyo katika miezi mitatu ijayo, na kuonya kuwa kama hali hiyo ikitokea, utakuwa ni msimu mbaya wa sita kwa nchi zinazoathiriwa zaidi ikiwemo Ethiopia, Kenya na Somalia.

Shirika hilo pia limesema ukame wa hivi sasa umeanza kufuatia hali duni ya mvua kutoka Oktoba hadi Disemba mwaka 2020 na umezidi kuwa mbaya kutokana na hali mbaya katika majira yote manne.