Waraka No. 1 wa China wasisitiza kujenga nchi yenye nguvu kubwa ya kilimo
2023-02-24 10:40:22| CRI

Hivi karibuni serikali kuu ya China ilitoa waraka No. 1 wa mwaka huu kuhusu suala la kilimo. Huu ni mwaka wa 20 mfululizo, ambapo China imetoa waraka No.1 kuhusu kilimo, na jambo ambalo linaonesha kuwa suala hili limepewa kipaumbele zaidi nchini China. Mwaka huu, kwa mara ya kwanza waraka huo umesema China itajenga nchi yenye nguvu kubwa ya kilimo.

China ina ustaarabu wa muda mrefu wa kilimo. Miaka elfu sita iliyopita, kilimo lilianza kustawi kwenye Bonde la Mto Manjano na Bonde la Mto Yangtze, na kilimo ndio chimbuko la ustaarabu wa Kichina. China ina watu bilioni 1.4, na kati yao takriban milioni 300 wanajishughulisha na kilimo, na kwa miaka mingi iliyopita, China imeshika nafasi ya kwanza duniani kwa utoaji wa nafaka, mboga, matunda, nyama, samaki na mazao mengine ya kilimo.

Hata hivyo, ikilinganishwa na sekta za viwanda na huduma ambazo zimeendelea kwa kasi katika miongo kadhaa iliyopita nchini China, kilimo bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tija ndogo ya nguvukazi vijijini, njia isiyofaa ya matumizi ya rasilimali, na uwezo mdogo wa ushindani katika soko la kimataifa.

Mwaka 2022, ripoti iliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa 20 wa  Chama cha Kikomunisti cha China iliweka lengo la kuijenga China kuwa nchi ya kisasa ya ujamaa yenye nguvu kubwa katika pande zote. Kilimo ndio msingi wa nchi yenye nguvu, na ili kufikia lengo hilo, China inapaswa kuendeleza kilimo kwa kuchukua hatua madhubuti.

Uamuzi wa China wa kujenga nchi yenye nguvu kubwa ya kilimo pia unatokana na mazingira ya kimataifa. Katika miaka ya hivi karibuni, hali ya kimataifa imebadilika kwa kiasi kikubwa, na suala la usalama wa chakula linafuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. China ni nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani, na ni muhimu kwake kuhakikisha usalama wa chakula. Hivi sasa teknolojia nyingi za hali ya juu za kilimo zinamilikiwa na nchi za magharibi. Katika siku zijazo, China itajitahidi kuendeleza kilimo, na kuboresha uwezo wake wa ushindani katika soko la kimataifa.

Ili kujenga nchi yenye nguvu kubwa ya kilimo, ni lazima kuongeza mapato ya wakulima. Juhudi za China za kupunguza umaskini imepata mafanikio makubwa, lakini umaskini vijijini bado haujaondolewa kabisa. Kutokana na waraka NO. 1 wa mwaka huu, pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, wakulima pia watapata faida zaidi kutoka kwa shughuli za kilimo, na kupewa haki za kutosha zaidi za kumiliki mali, ili kuimarisha mageuzi ya mfumo wa ardhi vijijini.