Siku ya wanyama pori ni muhimu sana duniani kwani katika hii huwa tunapata kusherehekea uzuri na maajabu ya mimea na wanyama pori waliomo ndani ya sayari yetu. Hivyo kila ifikapo Machi 3 huwa tunajaribu kukumbushana umuhimu wa viumbe hivi duniani. Kwa nini tunajali wanyamapori? Mbali na wajibu wa kimaadili wa kudumisha na kuiendeleza dunia, binadamu hutegemea bidhaa na huduma muhimu ambazo zinatokana na mazingira ya asili, kuanzia chakula na maji safi hadi udhibiti wa uchafuzi wa mazingira na uhifadhi wa hewa kaboni au ukaa.
Lakini cha kusikitisha ni kwamba hivi sasa mazingira ya asili na wanyamapori wako hatarini. Robo ya aina za wanyama zinakabiliwa na tishio la kutoweka, sababu kubwa ikiwa ni kuharibu karibu nusu ya ikolojia ambayo wanyama ndimo wanamoishi. Hivyo wakati umefika sasa na ni lazima tuchukue hatua ili kubadili mwelekeo huu. Na leo hii katika kipindi cha ukumbi wa wanawake, kuelekea maadhimisho haya ya siku ya wanyamapori duniani Machi 3 tutakuletea juhudi za wanawake katika kulinda wanyamapori.