ATMIS yachunguza ajali ya helikopta iliyosababisha vifo vya watu watatu nchini Somalia
2023-02-27 08:47:49| CRI

Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) imesema kuwa imeanza kufanya uchunguzi kuhusu mazingira yaliyosababisha helikopta yake ianguke Jumamosi kusini mwa Somalia, na kupelekea vifo vya abiria watatu waliokuwa ndani.

Tume ya AU imesema wakati helikopta yake ilipoanguka katika eneo la Baledogle, ilikuwa na maafisa 11 kutoka Jeshi la Kitaifa la Somalia na ilikuwa kwenye mafunzo ya pamoja ya mbinu za kuwahamisha majeruhi.

Kwa mujibu wa taarifa ya ATMIS iliyotolewa mjini Mogadishu, abiria watatu walipoteza maisha, na maafisa wanane waliojeruhiwa wamehamishwa Mogadishu kwa matibabu ya haraka.

Mwakilishi maalum wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia Bw. Mohammed El-Amine Souef amezifariji familia za marehemu na kuwatakia ahueni ya haraka maafisa waliojeruhiwa.