Msaada wa Marekani nchini Ukraine wafikia dola bilioni 50
2023-02-28 09:38:49| CRI

Shirika la habari la Interfax-Ukraine limetoa ripoti likimnukuu Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen baada ya mkutano wake na Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, kuwa Marekani imetoa msaada wa takriban dola za kimarekani bilioni 50 nchini Ukraine katika nyanja za usalama, uchumi, msaada wa kibinadamu na kijamii tangu kuanza kwa mzozo wa Russia na Ukraine.

Bi. Yellen alibainisha kuwa, Marekani imetoa dola za kimarekani bilioni 14 kusaidia uchumi wa Ukraine kuwa imara zaidi, na inapanga kutenga dola za kimarekani bilioni 8 kwa ajili ya mahitaji kama hayo katika siku za mbele.

Kwa upande wake, Bw. Shmyhal amesema kuwa mwaka 2022, Marekani ilikuwa mchangiaji mkuu wa fedha katika uchumi wa Ukraine kati ya nchi za kigeni. Kwa mujibu wa makadirio ya serikali ya Ukraine, nchi hiyo inahitaji ufadhili wa dola za kimarekani bilioni 38, ikijumuisha na vyanzo kutoka nje, ili kufidia nakisi ya bajeti mwaka huu.