Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani
2023-03-03 08:00:48| CRI

Tarehe 8 Machi kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ama Siku ya Wanawake Duniani. Katika siku hii, wanawake wanakutana na kujadiliana kuhusu mafanikio waliyopata katika sekta mbalimbali, changamoto wanazopitia, na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo. Kauli mbiu ya Siku hii mwaka huu ni “Dijitali: Uvumbuzi na Teknolojia kwa Usawa wa Jinsia.”

Kwa kaulimbiu hii, tunaweza kuona umuhimu wa ujumuishi wa wanawake katika masuala ya teknolojia na uvumbuzi, ili kuwawezesha kuendelea kutimiza ndoto zao katika nyanja mbalimbali. Mara nyingi wanawake wamekumbwa na unyanyasaji katika sehemu za kazi, biashara, elimu, na hata ndani ya ndoa. Ni wakati sasa kwa jamii kuungana kwa pamoja na kuhakikisha haki za mtoto wa kike na wanawake zinatimizwa, ni wakati sasa kwa wanawake na wasichana kupewa nafasi sawa na wanaume katika maeneo ya kazi, na ni wakati sasa kuona kuwa, mwanamke si kiumbe dhaifu asiyejiweza, bali kutambua kuwa, mwanamke na mtoto wa kike ni nguvu kubwa katika jamii, na anapopewa nafasi, anaweza kufanya mambo makubwa. Hivyo basi, katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii tutazungumzia mafanikio na changamoto wanazokutana nazo wanawake katika kutekeleza majukumu yao, ikiwa ni siku chache kabla ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka.