Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeeleza kuhitaji dola milioni 137 za kimarekani kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa nje na wa ndani milioni 3.3 katika Pembe ya Afrika, kutokana na ukosefu wa mvua katika misimu sita mfululizo unaoanzia mwezi Machi hadi Mei.
UNHCR imesema fedha hizo zitatumika katika kuwaokoa wakimbizi na watu waliolazimika kukimbia makazi yao kwa ajili ya kutafuta usalama na msaada, pia kusaidia jamii zinazowapokea. Kwenye taarifa yake Shirika hilo lilitoa wito kwa dunia kuwa na mshikamano na uungaji mkono zaidi, ili kulinda na kusaidia jamii zinazoathiriwa na ukame na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu.
Kwa mujibu wa Shirika hilo watu wanaokimbia makazi yao wanazidi kuongezeka huku mamilioni ya watu kutoka Somalia, Ethiopia na Kenya wakipigania maisha yao kutokana na uhaba wa vyanzo vya maji, njaa, kutokuwa na usalama na migogoro.