Mtu mmoja auawa katika maandamano nchini Sudan
2023-03-01 20:16:58| cri

Jeshi la Polisi nchini Sudan limesema, mtu mmoja ameuawa na askari polisi kadhaa kujeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika Khartoum, mji mkuu wa Sudan, jana jumanne.

Katika taarifa yake, Jeshi hilo limesema kifo cha mwandamanaji huyo kiliripotiwa katika Hospitali ya Nile Mashariki, wakati polisi wameanza kuchukua hatua za lazima kutambua masingira ya kifo hicho kupitia Mwendesha Mashtaka Mkuu.

Polisi wamewatuhumu waandamanaji kwa kutumia mabavu dhidi ya vikosi vya usalama, jambo lililosababisha kuchomwa moto kwa magari matatu ya polisi na majeruhi kwa askari polisi kadhaa.

Sudan imekumbwa na mgogoro wa kisiasa kuanzia Oktoba 25, 2021, wakati Baraza la Utawala la nchi hiyo na serikali kuvunjwa, na mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum na miji mingine imeshuhudia maandamano yanayodai kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini humo.