Rais Xi Jinping wa China alifanya mazungumzo na mwenzake wa Belarus Alexander Lukashenko jana Jumatano mjini Beijing.
Xi alisema mwaka huu ni mwanzo wa utekelezaji kamili wa kanuni elekezi zilizowekwa kwenye Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC, na mchakato wa maendeleo ya hali ya juu na ya kisasa utaleta fursa mpya kwa nchi nyingine ikiwa ni pamoja na Belarus.
Akisifu urafiki imara kati ya China na Belarus, Xi amesisitiza kwamba pande hizo mbili zinapaswa kuimarisha zaidi uaminifu wa kisiasa na China inathamini sana uungaji mkono thabiti wa Belarus kwa misimamo inayotambuliwa ya China katika masuala ya Taiwan, Xinjiang na Hong Kong, pamoja na haki za binadamu.
Kwa upande wake, rais Lukashenko alisema China ni mhimili mkuu katika kulinda amani ya dunia. Belarus inapenda kuimarisha uratibu na China katika masuala makubwa ya kimataifa na kikanda na kujitolea kwa pamoja kulinda usalama na utulivu wa kimataifa na kikanda.
Marais hao pia walibadilishana maoni kuhusu mgogoro wa Ukraine, ambapo Xi alisema kuwa msimamo wa China kuhusu mgogoro huo umekuwa thabiti na wazi, ambapo tayari imetoa waraka unaoeleza msimamo wake kuhusu utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo. Amesisitiza kuwa msimamo mkuu wa China ni kuunga mkono mazungumzo ya amani, akitoa wito wa kuzingatiwa kwa mwelekeo wa suluhu ya kisiasa, kuacha mtazamo wa Vita Baridi, kuheshimu ufuatiliaji halali kuhusu usalama, na kujenga muundo wa kiusalama wa Ulaya wenye uwiano, ufanisi na endelevu. Rais Lukashenko amesema nchi yake inakubaliana kikamilifu na kuunga mkono msimamo na mapendekezo ya China kuhusu utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Ukraine, ambao una umuhimu mkubwa katika kutafuta suluhu.