Mgombea wa chama tawala Tinubu ashinda uchaguzi wa rais Nigeria
2023-03-02 09:04:31| CRI

Tume ya uchaguzi nchini Nigeria imemtangaza Bola Tinubu kutoka chama tawala cha All Progressives Congress nchini Nigeria kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa Bw. Mahmood Yakubu amesema kuwa Tinubu amepata kura nyingi zilizopigwa wakati wa uchaguzi ambazo ni zaidi ya milioni 8.79.

Uchaguzi huo ni mmoja wa uchaguzi wenye ushindani mkali zaidi katika historia ya nchi hiyo. Rais huyo mteule mwenye umri wa miaka 70 alimshinda mpinzani wake wa karibu, Makamu wa Rais wa zamani Atiku Abubakar, ambaye ni mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha Peoples Democratic Party aliyepata kura zaidi ya milioni 6.98, akifuatiwa na Peter Obi wa chama cha Labor aliyepata kura takriban milioni 6.1.

Tinubu ambaye aliwahi kuwa gavana wa Jimbo la Lagos na seneta, alikuwa na nia ya kuwa rais kwa miaka mingi ambapo alijenga muundo thabiti wa kisiasa wenye mtandao mkubwa wa wafuasi nchini kote.