Benki ya Dunia kuunga mkono huduma za afya ya watoto nchini Tanzania
2023-03-02 23:47:01| cri

Benki ya Dunia na serikali ya Tanzania zimesaini makubaliano ya fedha kiasi cha dola za kimarekani milioni 579.93 katika mkopo mwepesi na msaada ili kuunga mkono huduma za msingi za afya ya watoto, upatikanaji wa maji safi katika maeneo ya vijijini, na miradi mingine ya afya nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Tanzania imesema, makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Waziri wa Wizara hiyo Mwigulu Nchemba na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete.

Taarifa hiyo imesema, fedha hizo zitasaidia mradi wa uwekezaji wa afya ya wajawazito na watoto, unaolenga kuboresha huduma muhimu za afya na upatikanaji wake, huku msisitizo zaidi ukiwa kwenye afya ya wamama wajawazito na watoto.