Mkurugenzi wa Kituo cha Elimu ya Afrika na China katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, David Monyae amesema, wakati China ikianza safari mpya ya kujenga jamii ya kisasa kwa pande zote, nchi zinazoendelea barani Afrika zinapaswa kutumia fursa inayotolewa na aina ya kisasa ya Kichina.
Akihojiwa na Shirika la Habari la China Xinhua, Bw. Monyae amesema kuibuka kwa China kuwa nguvu kubwa ya uchumi duniani kumeondoa mtazamo wa muda mrefu kuwa usasa wa kimagharibi ndio mfano halisi wa maendeleo. Ameeleza kuvutiwa kwake na mafanikio ya China katika kuondokana na umasikini uliokithiri na maendeleo ya kiuchumi katika miaka ya karibuni.
Monyae amesema, kitendo cha China kuondokana na umasikini uliokithiri ni mafanikio makubwa, kwa kuwa China imefanikiwa kutimiza lengo la kwanza la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2030 kabla ya muda uliopangwa.