China yakanusha kuziingiza nchi za Afrika katika mtego wa madeni
2023-03-06 21:55:35| cri

Wakati China ikikaribia kuadhimisha miaka 10 ya pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” (BRI), viongozi wake wameendelea kufahamisha pendekezo hilo kuwa si mtego wa madeni kwa Afrika kama inavyoelezwa na baadhi ya watu. Msemaji wa Bunge la Umma la China Bw. Wang Chao, amesema hadi sasa China imetoa zaidi ya dola za kimarekani trilioni 1 kama mikopo kwa karibu nchi 150 zinazoendelea, na kuwa mkopeshaji mkuu rasmi duniani kwa mara ya kwanza.

Bw. Chao, ambaye alikuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa China, amesema hadi sasa zaidi ya nchi 150 na taasisi zaidi ya 30 za kimataifa zimesaini makubaliano ya ushirikiano kupitia pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ambalo limekuwa na matokeo chanya kwa uchumi, ajira, na ustawi wa watu.

Amesema pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” halilengi maslahi ya kisiasa, na kwa mujibu wa takwimu kutoka taasisi za kimataifa kinachoitwa "mtego wa madeni," ni uzushi. Pia amesema kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, China si mkopeshaji mkuu wa Afrika, na karibu robo tatu ya deni la Afrika ni kutoka kwa taasisi za fedha na benki za biashara.