Naibu msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Farhan Haq amesema, kundi la waasi la M23 limepuuza makubaliano ya kusitisha vita yaliyoanza jana Jumanne katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Bw. Haq amesema, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres amesisitiza wito wake kwa M23 kuheshimu usitishaji vita ili kuweka mazingira ya kujiondoa kikamilifu na kwa ufanisi kutoka maeneo yote yanayokaliwa na kundi hilo mashariki mwa DRC. Pia amelaani ghasia zote dhidi ya raia na kusisitiza wito wake kwa makundi yote yenye silaha ya DRC na mataifa ya nje kuweka chini silaha zao na kusalimisha silaha bila masharti.