Kimbunga chasababisha vifo vya takriban watu 10 nchini Msumbiji
2023-03-08 21:34:12| cri

Shirika la Uratibu wa Misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA limesema takriban watu 10 wamefariki dunia kutokana na kimbunga cha Tropiki Freddy kilichotokea nchini Msumbiji, kinyume na ripoti za awali za mamlaka ya Msumbiji kwamba hakuna mtu aliyefariki.

Katika taarifa yake OCHA imesema imethibitisha vifo vya watu 11 katika nchi jirani ya Madagascar, ambapo zaidi ya nyumba 3,300 ziliharibiwa Jumapili iliyopita wakati kimbunga hicho kilipoikumba nchi hiyo.

Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa kimbunga hicho kinatazamiwa kupata nguvu ya kuwa kimbunga kwa mara nyingine tena, na wiki hii kinaweza kulikumba tena eneo la kati na kaskazini mwa Msumbiji. Kimbunga hicho ni moja ya vimbunga vilivyodumu kwa muda mrefu zaidi katika miongo ya hivi karibuni, kikivuka karibu Bahari yote ya Hindi kutoka pwani ya Indonesia hadi kusini mwa Afrika.