Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Bw. Mohamed Mchengerwa wiki ijayo atazindua boti ya kisasa itakayotumika kwa ajili ya utalii wa baharini katika Bahari ya Hindi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwapokea watalii milioni tano na kuleta mapato ya dola milioni 6 ifikapo 2025.
Amesema boti hiyo imetengenezwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport ya Tanzania na ina uwezo wa kuchukua watalii wapatao 50 kwa wakati mmoja.
Utalii wa baharini unaendelea kuimarika nchini Tanzania, hivi karibuni meli tatu zimetia nanga katika bandari tofauti za Tanzania zikiwa na watalii takriban 400 kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Meli zilizotia nanga ni pamoja na Corals Geographic Cruise iliyoleta watalii 120, Le Jaques Cartier-Ponant ya kupokea watalii 105 na Le Jaques Cartier-A & Luxury Expedition inayotarajiwa kutia nanga Machi 14, ikiwa na watalii 138.
Bw. Mchengerwa amesema boti hiyo iliyotengenezwa Tanzania ni miongoni mwa boti za kisasa zinazomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ikiwa na vifaa vya kisasa ili kuwapa watalii safari ya kukumbukwa.