Katika nchi nyingi, kilimo ni msingi wa uchumi, na wanaoshughulika na kilimo zaidi ni wanawake, hususan wale walioko maeneo ya vijijini. Kilimo ni uti wa mgongo wa mataifa mengi, lakini kwa bahati mbaya maendeleo katika sekta hiyo bado si mazuri. Teknolojia na mbinu za kilimo cha kisasa bado hazitumiwi na wakulima wengi, wengine kwa kutokujua, na wengine kwa kushikilia kilimo cha zamani, naweza kusema kilimo cha jembe.
Wanawake wanaoshughulika na kilimo wamepata mafanikio makubwa, lakini pia wamekumbana na changamoto mbalimbali. Kikubwa kinachowakwamisha wanawake hawa ni teknolojia ya kisasa ya kilimo, maana wengi wamezoea kilimo cha jembe na cha kutegemea mvua. Lakini hivi sasa sekta hii imekua na kupata maendeleo ya kasi, kuna zana nyingi za kilimo ambazo zinatumia teknolojia na hata droni. Kuna aina nyingi za kilimo ambazo mtu anaweza kufanya, hata kama ana eneo dogo la ardhi na kupata mavumo makubwa. Katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutazungumzia mchango wa wanawake katika sekta hii, mafanikio yao, na changamoto wanazopitia.