Maofisa wa Afrika wasema udijitali ni ufunguo wa kutimiza usawa wa jinsia na usalama wa chakula
2023-03-09 08:47:57| CRI

Maofisa wa ngazi ya juu wa Afrika wamesema, kutimiza usawa wa jinsia, usalama wa chakula na kuboresha huduma za afya kwa wanawake na wasichana barani Afrika kunategemea  uwekezaji endelevu katika teknolojia za kidijitali.

Kamishna wa Umoja wa Afrika kuhusu Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Buluu na Maendeleo Endelevu Josefa Sacko amesema katika hafla ya  kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani hapo jana, kuwa kuondoa pengo la jinsia katika upatikanaji wa teknolojia utaongeza mavuno ya mazao katika bara hilo kwa zaidi ya asilimia 20, na kupunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kwa asilimia 12.

Naye Katibu wa Idara ya Uwezeshaji wa Kiuchumi katika Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa Jemimah Njuki amesema, uwekezaji katika miundombinu rafiki, mafunzo na ujenzi wa uwezo ni ufunguo kwa kuhakikisha kuwa kuna usawa wa jinsia katika upatikanaji wa teknolojia muhimu kwa ajili ya kuboresha mnyororo wa thamani ya kilimo kwa bara la Afrika.