Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha waandishi wa Habari wanawake cha Tanzania TAMWA Bibi Rose Reuben, amesema jamii inatakiwa kuendelea kuibua changamoto zinazowakabili wanawake na watoto wa kike, kuelimisha umma kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, na kuwapongeza wanawake na watoto wa kike, waliofanya vyema katika jamii.
Bibi Rose Reuben amesema utafiti uliofanywa na taasisi ya Women at Web kwa kushirikiana na TAMWA, umebaini kuwa asilimia 79 ya wanawake wanasiasa na wanaharakati wa kisiasa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao wakati wa uchaguzi Mkuu.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa, uchaguzi mkuu wa 2020 umeonekana kama moja ya nyakati ambapo idadi kubwa ya wanawake katika siasa walikabiliwa na unyanyasaji wa mtandaoni.
Amesema ni dhahiri kuwa teknolojia imeleta neema, lakini wakati mwingine neema hiyo inatumiwa vibaya na kusababisha madhara kwa makundi mbalimbali hasa wanawake.