Naibu mjumbe wa China katika Umoja wa Mataifa, Balozi Dai Bing amesema, vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Sudan vimethibitishwa kuwa vimepitwa na wakati na vinapaswa kuondolewa.
Nchi wajumbe 15 wa Baraza hilo jumatano waliamua kwa kura 13 za ndio na mbili kutopiga kura, kuongeza muda wa Jopo la Wataalamu lenye jukumu la kuisaidia Kamati ya Vikwazo vya Baraza hili dhidi ya Sudan hadi Machi 12, 2024.
Akitoa maelezo kuhusu kura hiyo, Balozi Dai Bing amesema vikwazo vya Baraza hilo katika mkoa wa Darfur nchini Sudan, ambavyo vilianza mwaka 2004, vinalenga kumaliza mapigano ya kutumia silaha katika mkoa huo na kuisaidia Sudan kurejea katika amani na utulivu.
Ameongeza kuwa, Baraza la Mpito la Sudan na makundi ya upinzani yenye silaha wamesaini makubaliano ya amani ya Juba mwaka 2020, na Tume ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mkoani Darfur (UNAMID) ilimaliza jukumu lake na kuondoka mkoani Darfur mwishoni mwa mwaka huohuo.
Amesema Baraza hilo linapaswa kufanya tathmini za kila mara kuhusu vikwazo husika, na mara vigezo vinapofikiwa, vikwazo vinapaswa kubadilishwa ama kuondolewa kwa wakati.