Akikumbwa na umauti wa kusikitisha, rapa na mtunzi wa nyimbo kutoka Afrika Kusini Costa Titch alianguka na kufa kwenye tamasha la muziki huko Johannesburg. Msanii huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa akitumbuiza moja ya nyimbo zake, alipoanguka jukwaani. Baadaye, alisimama na kuendelea kutumbuiza, lakini alianguka tena na kufa.
Baada ya habari hizo kusambaa, wanasiasa kadhaa, wasanii, watu mashuhuri na watu wengine wametoa salamu za rambirambi akiwemo Julius Sello Malema, mbunge wa Bunge la Afrika Kusini. Tukio hilo lilitokea wakati Costa Titch alipokuwa akitumbuiza kwenye tamasha la muziki la Ultra Afrika Kusini lililofanyika jijini Johannesburg.
Video za mwimbaji huyo akicheza jukwaani dakika chache kabla ya kudondoka zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii. Katika mojawapo ya video hizo, iliyowekwa na mtumiaji wa Twitter, inaonesha mwimbaji huyo akinyanyuka mara baada ya kuanguka jukwaani mara ya kwanza na hata aliendelea kuimba. Baada ya sekunde chache, alianguka tena na hapo hakuweza kunyanyuka tena. Watu kadhaa waliojitolea walionekana wakienda kumsaidia baada ya tukio hilo. Chanzo cha kifo chake bado hakijajulikana kwa sasa.