Simba ‘Bob Junior’ auawa Serengeti
2023-03-16 19:03:34| cri

Simba maarufu Kaskazini mwa Tanzania aliyeishi katika Hifadhi ya Serengeti, ‘Bob Junior’ ameuawa Jumamosi iliyopita baada ya kushambuliwa na kundi la simba watatu waliokula njama kwa muda mrefu ya kuuangusha utawala wake.

Simba hao watatu waliowahi kujaribu kujisimika ufalme walilelewa na ‘Bob Junior’ tangu wakiwa wadogo lakini majaribio ya kufanya mapinduzi mara kadhaa ili kuuangusha utawala wa Bob Junior hayakufanikiwa na badala yake walikimbizwa katika maeneo hayo.

Simba ‘Bob Junior’ aliyejibebea sifa kwa kuwa mpole na anayekuwa na utulivu anapoona watalii, akisaidiana na kaka yake, Joel walitawala kwa zaidi ya miaka mitano na kuwa miongoni mwa Simba waliotawala kwa kipindi kirefu zaidi kabla ya kufanyika mapinduzi.

Mhifadhi Mwandamizi wa hifadhi hiyo, Fredy Shirima ameeleza kuwa tukio hilo ni asilia katika hifadhi lakini pia hutokea zaidi kwa Simba ambao hushikilia ngome dhidi ya wengine wanaoitaka. Bob Junior pia alikuwa na sifa za kipekee kama vile kuwa na manyoya mengi zaidi kuliko simba wengine lakini mwenye kuvutia kwa mwonekano na hutulia pale anapopigwa picha.

Wakati huohuo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) hivi saa linashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kumtafuta Simba ‘Joel’ ambaye amekimbia tangu kifo cha kaka yake ‘Bob Junior’. Hatua hiyo, inalenga kubaini hatma ya simba huyo mwenye umri wa miaka 12. Bw. Mwakilema alisema iwapo atapatikana amekufa, watakusanya mabaki ya Joel kwa nia ya kuuhifadhi mwili wake.