Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema makubaliano ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Saudi Arabia na Iran yaliyofikiwa chini ya upatanisho wa China ni fursa kwa kutatua migogoro nchini Yemen.
Mapema siku hiyo, mjumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Bw. Hans Grundberg alikaribisha makubaliano hayo kwenye ujumbe wake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema mazungumzo hayo na uhusiano mwema wa kijirani ni muhimu sana kwa kanda nzima na Yemen, ambapo pande husika lazima zitumie fursa hiyo vizuri ili kuelekea kwenye mustakbali wenye amani zaidi.
Yemen ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2014 wakati kundi la Houthi linaloungwa mkono na Iran lilishambulia miji kadhaa kaskazini mwa Yemen, na kulazimisha serikali ya Yemen iliyoungwa mkono na Saudi Arabia kuondoka mji wa Sanaa. Baadaye jeshi la muungano lilioongozwa na Saudi Arabia liliingilia kati mgogoro hiyo.