Vifo vya uzazi na wakati wa ujauzito
2023-03-24 08:00:14| CRI

Hivi karibuni Shrika la Afya Duniani (WHO) lilitoa ripoti yake likisema licha ya viwango vya vifo vya uzazi kupungua kwa theluthi moja katika miaka 20, mwanamke mmoja hufariki kila baada ya dakika mbili kutokana na ujauzito au matatizo ya uzazi. Viwango vilipungua sana kati ya 2000 na 2015 lakini vilidorora kwa kiasi kikubwa kati ya 2016 na 2020, na katika baadhi ya mikoa hata vimebadilika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, ni ajabu na kweli kwamba uzoefu unaotakiwa wa matumaini chanya umegeuka kuwa shubiri na machungu kwa wanawake wajawazito. Kwa ujumla, idadi kubwa ya vifo imesalia katika nchi maskini zaidi duniani na zile zilizoathiriwa na mizozo.

Mathalani mwaka 2020 takribani asilimia 70 ya vifo vya wajawazito vilitokea katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara. Nchi 9 zinazokabiliwa na majanga ya kibinadamu viwango vya vifo vya wajawazito vilikuwa zaidi ya maradufu ya wastani wa vifo duniani ambapo ni vifo 551 katika kila vizazi 100,000 ikilinganishwa na wastani wa dunia ambao ni vifo 223 kwa kila vizazi 100,000. Hivyo kufuatia tatizo hilo kuongezeka hasa katika nchi za Afrika leo kwenye kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutazungumzia vifo vya uzazi na wakati wa ujauzito, na bahati nzuri pia tumempata Dkt Elizabeth ambaye tutaongea naye baadaye.